![]() |
| Askari wakizinga waandishi ili wasimpige picha mtuhumiwa wa mauaji ya Mwangosi |
Njama za kumtorosha askari Pasificus Cleophace Simon mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten Daud Mwangosi mwenye namba G2573 zinazofanywa na jeshi la polisi zimebainika.
Mtandao huu umegundua njama hizo kutoka ndani ya jeshi hilo ikiwa ni siku moja baada ya mtuhumiwa huyo kupandishwa kizimbani.
Septemba 12, 2012 siku aliyofikishwa mtuhumiwa huyo mahakamani, majira ya saa 10:47 jioni katikia Grocery moja ndani ya jengo la Iringa Net jirani na benki ya Posta, mtandao huu umekariri mazungumzo ya vijana wanne wanaoaminika kuwa ni askari wa kikosi cha kutuliza ghasia katika mkoa wa Iringa waliokuwa wamevaa kiraia wakisema dawa kubwa ya kumnusuru askari mwenzao ni kumkimbiza nje ya nchi vinginevyo hana utetezi.
“Tumejaribu kwa kila njia kufikiria jinsi ya kumnasua mwenzetu tukaona hakuna, ila tumekubaliana kuwa afikishwe mahakamani ili asomewe mashtaka yake kama kawaida huku tukifanya mpango wa kumkimbiza nje ya nchi halafu baada ya kufanikisha tunaiambia mahakama kuwa mtuhumiwa ametoroka” alisema mmoja wa vijana hao.
Katika mazungumzo hayo wakaeleza kuwa kinachotakiwa ni ofisi za uhamiaji kuharakisha pasi ya kusafiria ili asiendelee kuhudhuria mahakamani kwa muda mrefu.
“Anayeshughulikia pasi ya kusafiria anatakiwa afanye haraka ili mtuhumiwa asihudhurie mahakamani kwa muda mrefu” alisema mmoja.
Wakati hayo yote yakizungumzwa ndani ya Grocery hiyo wakidhani wapo wenyewe tu, mmoja alisema kuwa IGP Said Mwema asingekubali mbinu hiyo kutumika, askari hao walikuwa tayari kulipuana ili kuhakikisha na yeye anakuwa miongoni mwa watuhumiwa.
“IGP Mwema alitumia busara kufanya hivyo vinginevyo kule ndani kusingekalika. Ungekuwa ni uonezi mkubwa kama mwenzetu atiwe gerezani wakati alikuwa akitii amri yao wenyewe. Inabidi lifanyike haraka iwezekanavyo ili hata Kamanda Kamuhanda aondoke maana wananchi wameshapata hasira usione wamekaa kimya ipo siku lolote linaweza kutokea” alisema mmoja wao.
Wakati mtandao huu ukibaini hayo, chanzo kingine cha kuaminika kutoka ndani ya jeshi hilo kimetoa taarifa kwa siri kuwa kuna njama za kumtorosha mtuhumiwa wa mauaji kwa kuwa jeshi limeshindwa namna ya kumsaidia mtuhumiwa.
Chanzo ambacho hata hivyo kilitoa taarifa kwa masharti ya kutaka jina lisiandikwe kimesema mtuhumiwa yupo katika wakati mgumu kwa kile kilichoelezwa kuwa jeshi limeshindwa namna ya kumsaidia huku kikisema kuwa hata kamanda Michael Kamuhanda anatakiwa kuwajibishwa kwa kuwa yeye ndiye aliyetoa amri.
“Tulikaa na kamanda Kamuhanda tukamueleza kuwa askari mwenzetu hawezi kupelekwa mahakamani bila yeye kuwajibika kwa kuwa ndiye aliyetoa amri na mauaji yakatokea. Baada ya malumbano kutofika mwafaka, ilibidi IGP Mwema afike. Tuliongea na Mwema siku mbili ikaonekana Kamuhanda hakwepi kesi hiyo. Ili kumlinda Kamuhanda, Mwema alipanga mbinu ya kumkimbiza mtuhumiwa njea ya nchi akamshawishi askari anayetuhumiwa akakubali ndipo tukaridhia” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilieleza kuwa kama mbinu hiyo isingetumika, kesi hiyo ingekuwa na mnyororo mkubwa wa watuhumiwa kwa sababu mtuhumiwa angeongea aliyemtuma ndipo hapo ungeanza mlolongo wa wahusika.
![]() |
| Aliyejifunikia kofia ndiye mtuhumiwa |
“Hii kesi ina watu wengi na isingekuwa hii mbinu inayotaka kutumika kumtorosha mtuhumiwa ili kesi ipotee, Kamuhanda na wengine wamo kujibu tuhuma kwa sababu yule kijana hatakubali kutumikia jela pekee yake wakati haukuwa uamuzi wake” kilisema chanzo hicho.
Kikitoa ufafanuzi juu ya askari waliozuia kwa kuwasukuma waandishi wahabari wasimpige picha mtuhumiwa huyo mahakamani, kilisema kuwa ile ni mbinu iliyopangwa toka ndani ya kikao kilichofanyika na Mwema ili mtuhumiwa asijulikane sana kwa watu.
“Tulipokuwa kwenye kikao na Mwema hilo lilizungumzwa kuwa askari wanaompeleka mtuhumiwa mahakamani wahakikishe wanamlinda kwa kila njia ili asipigwe picha kwani akijulikana sana sura yake hata huko atakakopelekwa anaweza kukamatwa tena; utakumbuka jinsi walivyokuwa wakifanya askari mahakamani kuzuia asipigwe picha, zile ni mbinu ambazo zimetolewa mafunzo kabisa” kilisema chanzo chetu.
Ilielezwa kuwa tayari mtuhumiwa amekwisha kutengenezewa cheti kingine cha kuzaliwa kwa jina la Kacian Alphonce Mapila huku akielezwa kuwa ni Mhehe tofauti na kabila lake (Mhaya).
“Si kwamba kinachoelezwa hapa ni propaganda, tayari amekwisha kutengenezewa jina lingine kwa ajili ya kutengenezewa hati ya kusafiria kwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji haruhusiwi kupewa hati ya kusafiri kwenda nje. Jina jipya alilotengenezewa ni Kacian Alphonce Mapila na kabila lake jipya ni Mhehe” kilisema chanzo hicho.
Insekta Mkuu wa Polisi Said Mwena alifika Iringa 8 Septemba kwa ajili ya mazungumzo na askari wa Iringi aliyofanyika latika ukumbi wa kituo kikuu cha Polisi kilichopo mkabala na Soko Kuu la Manispaa.
Baada ya mazungumzo yake na askari, Mwema angefanya kikao na viongozi wa madhehebu ya dini laki hakufanikiwa kuonana nao kutokana na sababu inayosemekana kuwa viongozi hao waligoma.
Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zieleza kuwa Mwema alikuwa na nia ya kuomba radhi kwa viongozi wa dini juu ya mauaji yaliyotokea Morogoro na Iringa na sehemu zingine na kuhusisha jeshi la polisi lakini viongozi hao walikacha kumsikiliza.
Mwema aliondoka Iringa 11 Septemba asubuhi baada ya juhudi za kuonana na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali kushindikana.


No comments:
Post a Comment