| IGP Said Mwema |
Katika mawazo yangu finyu nilikuwa nikifikiri watu wanene, wenye matumbo makubwa, kipara na wenye sura nzuri ndiyo wenye akili kuliko watu wengine wote.
Siku moja kukawa na mkutano wa hadhara katika kijiji fulani, wakati wa mkutano ule watu wakawa wananyosha mikono kwa ajili ya kuuliza maswali. Miongoni kwa watu hao waliokuwa wakinyosha mikono kulikuwa na mtu mnene na mwingine alikuwa na kipara.
Mawazo yangu yakawa pale pale kwamba mnene na mwenye kipara ndio wanaostahili kuuliza maswali kumbe mawazo hayo hayakuwa ya kwangu pekee yangu.
Mwenyekiti wa kijiji hicho naye alionekana kuwa na mawazo ya kwangu kwa kuwa alikuwa akitoa nafasi kwa watu ninaowafikiria mimi tu ndipo nikaamini kuwa sikuwa nafikiri kumbe nilikuwa sahihi kwa mawazo yangu.
Baada ya muda mkutano unapoelekea mwishoni kijana mmoja alisimama kwa kulazimisha na kumuuliza Mwenyekiti wa kijiji hicho akisema “ndugu Mwenyekiti, ulitumia vigezo vipi kuwapatia hawa watu nafasi ya kuuliza maswalia katika mkutano huu?”. Mwenyakiti alishikwa na butwaa na kukosa cha kujibu akauliza swali, “we kijana unamaana gani na swalia lako?”. Kijana akasema “nimekuwa nikikuangalia kwa muda wote kila siku ya mkutano unawapa hao hao tu nafasi ya kuuliza maswali; “kwani sisi hatuwezi?”.
Mwenyekiti huyo kwa ghadhabu akasema “kwani wewe ulitaka kusemaje?” Kijana huyo akasema “watu waliokuchagua wewe waliangalia vigezo gani? Nimeuliza hivyo kwa sababu kiongozi kama wewe hutakiwi kuwa na upendeleo wala ubaguzi lakini wewe umekuwa ukionesha upendeleo wa moja kwa moja bila kupita mlango wa nyuma” alisema kijana huyo.
Kutokana na maswali yaliyokuwa yakiulizwa na kijana yule wakati ule, nilikuwa nikifunguka taratibu na baadaye nikapata jibu kuwa sikuwa sahihi nikabadilisha mawazo yangu nikaamini usemi mmoja usemwao “ukubwa wa pua si wingi wa kamasi”.
Kutokana na mtizamo huo linakuwa ni jambo la aibu na la kushangaza kama mtu amefuga kuku nyumbani kwake halafu akitaka kumchinja anaamua kutumia bunduki.
Hii ni sawa na jeshi la Polisi nchini kutumia silaha za moto kwa wananchi wasio na silaha wala hawajapata mafunzo ya kijeshi wala mazoezi ya kucheza mchezo wa rede.
Kila linapojitokeza tatizo linalohusiana na jeshi la Polisi kila wakati jeshi hilo limekuwa likijitoa kutokuhusika na tukio huku wakishindwa kuwakamata wanaofikiri wao ndio wahusika.
Walipouawa watu Arusha jeshi hilo lilijitoa katika tukio hilo na kuwatuhumu viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kuwa ndio waliohusika jambo ambalo kwa akili ya kawaida kabisa kauli hizo zinaonekana ni za kitoto.
Wakati CHADEMA wanafanya operesheni yao katika Mkoa wa Morogoro, mtu mmoja aliuawa na risasi bila ya kuwa na hatia na Polisi kudai kuwa alipigwa na kitu kizito kilichorushwa na raia bila kutaja ni kitu gani na mrushaji ni kama amekamatwa.
Historia hii bado inanikumbusha zile fikra zangu za awali kuwa watu wanene, wenye kipara, sura nzuri na wenye matumbo makubwa ndiyo wenye akili.
Kuuawa kwa Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Iringa (IPC) na mwandishi wa habari katika kituo cha Televisheni cha Chanel Ten Daud Mwanosi, bado kunanipa mwanga zaidi kuwa mawazo yangu yalikuwa ya giza badala ya nuru.
Kutokana na kifo hicho Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linatoa kauli ya kujiondoa kabisa na tukio hilo na kuwabebesha wananchi tuhuma kuwa ndio waliorusha bomu hilo . Wakati Jeshi hilo likitoa kauli hiyo limeshindwa kueleza kuwa mwananchi aliyerusha bomu hilo amekamatwa, limeshindwa kueleza ni kwa nini bomu hilo likamuua mwandishi huyo pekee wakati mwandishi huyo alikuwa ameshikiliwa na moja ya askari hao.
Kwa hali ya kawaida tu nilitegemea kwa kuwa jeshi la Polisi linaonekana wazi kushindwa kutumia akili na kutumia nguvu, mfumo wa jeshi hili ungebadilishwa na wale wenye dhamana ambao hulipwa kodo za watanzania kwa ajili ya kufanya kazi hizo za usalama.
![]() |
| Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete |
Kuna usemi mmoja una sema “mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo”. Mtunzi wa usemi huu aliangalia mbali sana kwani maana ya usemi huu inajionesha wazi katika maisha ya kila siku ya mwanadamu hususani watu wa nchi hii.
Mfumo wa jeshi hili unashindikana kubadilika kwa sababu wenye dhamana ndiyo walezi wenyewe kwa sababu hiyo hawana mawazo tofauti na wale wanaoshindwa kufanya kazi wanazotakiwa kufanya kwa manufaa ya taifa na kufanya kazi za kijambazi.
Kifo cha Mwangosi ni cha kijambazi kwa kuwa aliyehusika na tukio hilo hakika ana harufu zote za ujambazi. Hii inaonesha kuwa nchi inataka kuwa ya kijambazi badala ya kidemokrasia.
Naamini nchi yoyote duniani inaendeshwa kwa sheria na kanuni na pindi mtu yeyote anapovunja sheria na kanuni hizo huchuliwa hatua na kupelekwa kwenye vyombo husika ili aweze kuelekezwa makosa yake kuwa amevunja utaratibu kadiri ya taratibu husika.
Badala ya kufanyika hivyo, Jeshi la Polisi nchini limeona hakuna haja ya kuwepo mahakama amabayo ni moja ya mihimili ya taifa na kuona wao ni suluhu ya kila kitu. Ni njia zipi watatumia kujinasua jeshi la Polisi kwa unyama uliofanyika kwa Mwangosi? Ni mtu wa aina gani ataamini taarifa za jeshi la polisi kujitoa katika tukio hilo ?
Hata angekuwa mwanangu wa miaka 4 hawezi kushawishiwa na taarifa zozote zitakazoliondoa jeshi la Polisi katika tukio hilo vinginevyo aoneshwe raia aliyerusha bomu likamuua Mwangosi na kuueleza umma kuwa alilipata wapi na pia kioneshwe kitu kizito kilichorushwa na raia kikamuua mwanachi kule Morogoro pamoja na kukamatwa kwa raia huyo ili ajibie suala hilo.
Waswahili wanasema, “tabia ni ngozi”. Ngozi yoyote ile ni asilia lakini kwa kutumia kemikali au kitu chochote kwa madhumuni ya kuibadilisha, huiharibu badala ya kuitengeneza.
Kwa matukio haya yote kwa upande wangu sioni haja ya uwepo wa IGP wala Wizara ya ulinzi na usalama pamoja na Waziri wa wizara hiyo.
Nchi za kidemokrasia yakitokea matatukio ya kinyama kama haya, waziri wa ulinzi na usalama, kamanda wa polisi nchini IGP huachia ngazi wenyewe bila kusulutishwa.
Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18 inatoa haki kwa kila mtu kupata na kutoa habari bila kikomo cha mipaka ya nchi. Kuuawa kwa Mwangosi kunakwenda tofauti na ibara hiyo.
Sipendi sana kuandika kwa hisia lakini kutokana na ukweli wa waandishi waliokuwapo katika tukio la kuuawa Mwangosi nina kila sababu ya kusema jeshi la Polisi halijawatendea haki wananchi kwa kuwanyika haki yao ya kupata habari.
Nina kila sababu ya kuwataka IGP Said Mwema pamoja na Waziri wa ulinzi na usalama wajiondoe kwenye nafasi zao kwa kuwa wanaonesha dalili zote kuwa wameshindwa kuwatumikia wananchi.
Mwangosi alikuwa mlipa kodi ambazo wao hupewa kama mshahara. Leo hii maaskari hao walipwe nini kama walipa kodi hawa wameuawa na jeshi hilo ? Waswahili husema, “usipoziba ufa , utajenga ukuta”. Huu ndio mtizamo wangu kuwa njia pekee ya kumaliza suala hili ni hao watu kuachia nafasi zao kwa kushindwa kuwalinda wananchi na kuwasababishia kuishi maisha ya wasiwasi kama wakimbizi ndani ya nchi yao .
Jeshi la polisi limeshindwa kulinda haki za binadamu na kuendelea kufanya unyama na udhalilishaji kwa kuwafananisha binadamu na wanayama wengine. Tukio alilofanyiwa Mwangosi ni la aibu mbele ya utu wa mwanadamu na niudhalimu mkubwa.
Tendo hilo linaonesha dalili zote za mawazo yangu finyu ya hapo awali kuwa watu wanene, wenye kipara, wenye sura nzuri na wenye matumbo makubwa kuwa ndiyo wenye akili kwani inaonesha kumuweka mtu kama huyo katika nafasi asiyoweza kuimudu kunatokana na mawazo hayo na upendeleo wa hali ya juu.

No comments:
Post a Comment